Alizeti haitoi mailisho pekee, pia inatoa
mafuta bora kwa afya ya binadamu na pia malighafi inayotumiwa na nyuki
kutengeneza asali.
Unapotengeneza chakula cha mifugo peke yako, si tu kupunguza gharama,
lakini pia inakupa uhakika wa kuwa na chakula bora. Pia Wafugaji wa
nyuki wanaopanda alizeti wanapata faida ya ziada kwa kupata asali iliyo
bora kwa sababu nyuki hukusanya poleni kutoka kwenye alizeti wanapofanya
ushavushaji.
Chanzo kizuri cha protini
Chakula cha mifugo kinachotengenezwa kutokana na alizeti ni chanzo
kizuri cha protini kwa ajili ya mifugo, hasa ng’ombe wa maziwa, kuku,
nguruwe na hata sungura. Malisho haya yana kiasi kikubwa cha protini,
nyuzi nyuzi na kiasi kikubwa cha mafuta. Malisho haya yana protini kiasi
cha asilimia 29-30, kiasi cha nyuzi nyuzi asilimia 27-31.
Moja ya tabia nzuri ya alizeti ni kwamba haina vitu vinavyoathiri
virutubisho kwa mifugo, hata hivyo, ina kiasi kikubwa cha nyuzi nyuzi na
mashudu yake kuwa magumu kiasi, jambo ambalo husababisha ugumu kidogo
kwenye kusagwa tumboni. Mbali na virutubisho vya aina nyingine, alizeti
ni chanzo kizuri cha kalishamu, fosiforasi na vitamini B.
Ubora wa alizeti inayotumika kwa ajili ya malisho ya mifugo inategemeana
na namna ambayo imetayarishwa. Kwa mfano, alizeti inayosagwa bila
kuondoa maganda ya nje, ina kiasi kikubwa cha nyuzi nyuzi (kati ya
asilimia 27-30, lakini inakuwa na kiasi kidogo cha protini asilimia 23).
Alizeti ambayo imetayarishwa kwa ubora wa hali ya juu huwa maganda
yameondolewa na inakuwa na kiasi kikubwa cha protini, kiasi cha asilimia
40.
Mkulima anapaswa kufahamu kuwa alizeti bado inakuwa na virutubisho hata
kama haitatayarishwa kwa ustadi. Mfugaji anaweza kutumia soya na karanga
badala ya alizeti, lakini ni lazima apeleke alizeti kupima kuhakikisha
kuwa ina nyuzinyuzi na virutubisho kwa kiwango cha nyuzinyuzi na protini
kinachokubalika.
Inapendekezwa kutumia alizeti
Kulingana na utafiti ambao umefanyika nchini Tanzania, alizeti
iliyochanganywa na pumba ya mahindi kwa kiasi cha asilimia 30, kisha
kulishwa ng’ombe aina ya Zebu ina uwezo wa kuongeza uzalishaji wa maziwa
kutoka lita 6.6 kwa siku mpaka lita 8.1 kwa siku. Nchini Zimbabwe,
mashudu ya alizetu huchanganywa na mahindi pamoja na mabua ya mahindi
ambayo yamewekwa urea kwa kiwango cha wastani wa kilo 4.4 kwa siku, na
kulishwa ng’ombe aina ya Jersey pamoja na ng’ombe chotara ambao hulishwa
katika machungo ya wazi, Ng’ombe hawa huongeza kiasi cha maziwa kwa
wastani wa kilo 5.8 mpaka kilo 6 kwa siku.
Aina ya alizeti
Kuna aina mbili za alizeti, alizeti fupi na alizeti ndefu. Aina ndefu
hurefuka mpaka kufikia kiasi cha urefu wa mita 1.5-2.4. Uzalishaji wake
ni hafifu ukilinganisha na mbegu za kisasa. Aina hii mara nyingi huwa
ile inayojulikana kama Hungary nyeupe na Fedha. Alizeti fupi ni
inayotokana na mbegu za kisasa ambayo huwa na urefu wa mita 1.2, aina
hii huwa na mavuno mazuri zaidi ukilinganisha na aina ndefu.
Kutengeneza chakula cha mifugo
Kilo tatu na nusu za alizeti inapokamuliwa hutoa mafuta lita moja na mashudu kilo mbili na nusu.
Resheni kwa ng’ombe wa maziwa
•Changanya kilo 18 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi ili kutengeneza chakula cha ng’ombe.
•Mlishe ng’ombe anaezalisha maziwa kwa wingi kiasi cha kilo 4 ya
mchanganyiko huo na kilo 2 kwa ng’ombe anaezalisha kiasi kidogo cha
maziwa.
•Mbali na kulisha mchanganyiko huo, ng’ombe wa maziwa ni lazima apewe
kiasi kingine cha chakula cha kawaida cha kila siku kama vile matete,
hay, au aina nyingine yoyote ya malisho bora kwa kiasi cha kutosha.
Resheni kwa ajili ya kuku
Chakula cha kuanzia: Changanya
kilo 22 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za pumba ya mahindi Chakula
cha kukuzia: Changanya kilo 20 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za
pumba ya mahindi au chenga.
Chakula kwa ajili ya kuku wanaotaga: Changanya kilo 18 za mashudu ya alizeti na kilo 100 za chenga za mahindi
ZINGATIA: Unapotengeneza chakula
kwa ajili ya ng’ombe wa maziwa, mfugaji ni lazima ahakikishe kuwa
mashudu hayazidi asilimia 20 ya resheni ya kulishia. Kwa ajili ya
kulishia kuku, alizeti isizidi asilimia 7 ya jumla ya resheni.
Namna ya kuzalisha alizeti
Hali
ya hewa: Alizeti hustawi vizuri zaidi kwenye udongo tifutifu, wenye
rutuba ya kutosha. Zao hili lina mizizi inayoenda chini kwa kiwango cha
kikubwa hivyo kuiwezesha kustawi hata katika sehemu yenye kiwango kidogo
cha mvua. Kiasi cha wastani wa milimita 500-750 za mvua zinatosha
kabisa kwa uzalishaji wa alizeti. Inaweza kulimwa kutoka usawa wabahari
mpaka kufikia mwinuko wa mita 2600 kutoka usawa wa bahari.
Maandalizi ya shamba
Ni lazima kuhakikisha kuwa shamba limelimwa vizuri, ili kuweza kupata sehemu nzuri ya kusia mbegu.
Nafasi: Mbegu zinaweza kupandwa
kwa nafasi ya sentimita 75 kwa 30 kwa kiasi cha kilo 2 kwa ekari moja
(sawa na kilo 5 kwa hekari). Panda mbegu 3 kwa kila shimo, kisha acha
mmea mmoja kwa kila shimo mimea inapofikia urefu wa sentimita 10-20.
Matumizi ya Mbolea
Alizeti hufanya vizuri kwenye udongo wenye rutuba. Matumizi ya mbolea
inayotokana na miamba aina ya fosifeti inafaa zaidi kwa kuwa alizeti
inahitaji fosifeti kwa kiasi kikubwa. Matumizi ya mbolea mboji
iliyoandaliwa vizuri itaongeza virutubisho vya ziada kwenye udongo.
Alizeti hukua vizuri katika sehemu isiyokuwa na magugu. Palilia alizeti inapokuwa na urefu wa mita 0.7 (Kiasi cha wiki 4).
Ndege waharibifu
Ndege wanaweza kuharibu kiasi cha asilimia 50 ya alizeti endapo
hawatafukuzwa. Ili kuzuia uharibifu huo, mkulima anaweza kuchukua hatua
zifuatazo;
•Vunja shina la alizeti kufikia usawa wa magoti kabla ya alizeti
kukauka. Unaweza pia kuvunja katika urefu wowote lakini alizeti iangalie
chini ili kuzui ndege kudonoa.
• Ondoa alizeti shambani baada ya kukauka na kuihifadhi.
• Ubanguaji unaweza kufanyikia nyumbani kwa kutumia fimbo
• Alizeti ni lazima ikaushwe mpaka kufikia kiwango cha unyevu wa asilimia 10 kabla ya kuhifadhiwa
0 comments: