Mipango thabiti huleta mafanikio katika ufugaji
wa ng’ombe wa maziwa. Wafugaji waliofanikiwa wanafahamu fika kuwa
katika uzalishaji wa maziwa 20% inatokana na aina ya ng’ombe na 80%
matunzo.
Tumekutana
na kupokea maombi kutoka kwa watu wengi ambao wanataka kuanzisha
ufugaji wa ng’ombe, lakini hawajui ni wapi pa kuanzia. Kwa kawaida, wao
wanaweka pesa, kutafuta ng’ombe, kununua na mwisho hupata ng’ombe. Hapo
ndipo kuhangaika na kupata msongo wa mawazo kwa mfugaji huanza kwa kuwa
ng’ombe hazalishi maziwa kutokana na aina yake pekee.
Kwa wafugaji wadogo walio wengi, wakati ambapo ng’ombe anafika zizini
kwake wanakuwa bado hawajawa tayari kumpokea ng’ombe huyo kwa ajili ya
ufugaji. Ili ujasiria mali kwa njia ya ng’ombe uweze kufanikiwa na
kumfaidisha mfugaji kiuchumi, mfugaji ni lazima ahakikishe kuwa miundo
mbinu muhimu inakuwa tayari kabla ya kumleta ng’ombe.
Kwa mujibu wa mwongozi wa kitabu cha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa Afrika
ya mashariki, ng’ombe wa maziwa ni lazima wapate mahitaji yafuatayo:
• Malisho bora na maji safi ya kunywa
• Afya bora bila majeraha
• Mazingira safi ikiwa ni pamoja na banda lililojengwa vizuri
• Uangalizi mzuri na wa kirafiki, ambao humfanya ng’ombe kuwa mtulivu bila kuwa na msongo.
Bila mahitaji haya muhimu, na mfugaji kutokumtunza ng’ombe vizuri,
asitegemee kuwa ng’ombe huyo atazalisha kiwango kizuri cha maziwa.
Uzalishaji wa kiwango cha maziwa na ubora wake unategemeana kwa kiasi
kikubwa na mambo hayo yaliyotajwa hapo juu. Wataalamu wanasema kuwa 20%
ya uzalishaji wa ng’ombe inatokana na aina ya ng’ombe na 80% matunzo
kutoka kwa mfugaji. Muhudumie ng’ombe wako vizuri naye atarudisha kwa
kuzalisha maziwa vizuri.
Mipango
Wafugaji ni lazima wawe na mipango thabiti kwa ajili ya ufugaji wa
ng’ombe. Hii hujumuisha idadi ya ng’ombe mfugaji anayotaka kufuga,
pamoja na kufahamu ni kiasi gani cha malisho kinachohitajika kwa kipindi
chote cha mwaka. Mfugaji pia anapaswa kufahamu kuwa ni kwa namna gani
malisho yanafaa kutolewa kwa wanyama.
Mfugaji ni lazima pia apange ni kwa namna gani atapata malisho kwa
kipindi chote. Hii inamaanisha kuwa ni muda gani atapanda, kuvuna na
kuhifadhi. Mipango ni nguzo muhimu sana kwa kuwa inawezesha kusaidia
kufahamu ni nini cha kufanya, namna ya kufikia malengo yaliyokusudiwa,
na ni hatua gani imefikiwa. Mfugaji ambaye hana mipango thabiti ni sawa
na mtu anayeanza safari bila kufahamu mwisho wa safari yake ni wapi.
Mahitaji ya mlo kamili
Shughuli ya ufugaji wako itakamalika siku ambayo utaweza kuelewa
uhusiano kati ya ulishaji wa ng’ombe, uzalishaji wa maziwa na mapato.
Endapo ng’ombe wa maziwa atalishwa kwa malisho hafifu ni dhahiri kuwa
uzalishaji wa maziwa pia utakuwa hafifu.
Malisho bora
Tafuta ni aina gani ya malisho hufanya vizuri katika ukanda wako.
Malisho endelevu hutegemeana kwa kiasi kikubwa na aina ya malisho na
utunzaji wake shambani mwako. Chukulia kuwa wewe ni mfugaji mdogo na
hauwezi kumudu gharama za umwagiliaji, ni lazima utumie kwa kiasi
kikubwa malisho ya wakati wa mvua na kuhifadhi ili kuweza kuyatumia
wakati wa kiangazi.
Inashauriwa kupanda majani ya malisho kwa kiasi kikubwa uwezavyo wakati
wa mvua. Wahamasishe majirani zako kupanda malisho pia, ili baadaye
uweze kununua kutoka kwao. Matete, nyasi, majani ya mtama, majani ya
mahindi, lusina, desmodiamu, na alizeti ni miongoni mwa malisho ambayo
hufanya vizuri katika maeneo mengi nchini Tanzania.
Kiwango cha kutosha
Fahamu ni kiwango gani kinachotosha kwa kila ng’ombe wako. Hii
itakusaidia kufahamu ni kiasi gani cha malisho upande na ni kiasi gani
uhifadhi. Kwa wastani, ngombe wa maziwa aliyekomaa mwenye uzito wa kilo
400, anayefugwa ndani ana uwezo wa kula kilo 12 za majani makavu kwa
siku. Kumbuka kuwa endapo mifugo yako haitapata malisho ya kutosha
wataonesha kwa muonekana wao, na kisha kukupa adhabu kwa kuzalisha
maziwa kidogo sana. Kama kanuni inavyoeleza, hakikisha kuwa 15%-18% ya
malisho yote ni protini.
Zingatia utunzaji na uzalishaji wa malisho vizuri
Wafugaji walio wengi hukwepa kupanda majani ya malisho kwa kuogopa
gharama ya mbolea na mbegu. Kwa uzoefu wetu mfugaji anaweza kutumia
mbolea inayotokana na wanyama kupanda malisho na kuyatunza vizuri.
Matete ni moja wapo ya malisho hayo. Endapo malisho hayo yatawekwa
mbolea vizuri, shamba dogo tu la malisho linaweza kukupatia malisho ya
mifugo kwa kipindi chote cha mwaka.
Weka malisho katika hali ya usafi
Hifadhi malisho katika sehemu nzuri, sehemu ambayo hayatapigwa na jua
moja kwa moja, mvua au kuwepo uwezekano wa vitu vingine vinavyoweza
kuyaharibu kama vile siafu na wadudu wengineo. Majani ya malisho ni
lazima yanyaushwe vizuri kuepuka viini vya sumu vinavyoweza kuwepo
kwenye malisho. Mfugaji anaweza kuamua juu ya ubora wa malisho kutokana
na muonekano wake, harufu na mguso. Malisho mabichi yenye wingi wa
majani kuliko shina, yenye kijani kilichokolea, na ambayo yana mguso
nyororo, ni moja ya malisho bora ukilinganisha na yale yenye ugumu,
shina kubwa na rangi ya njano. Epuka kulisha mifugo yako kwa kutumia
malisho yenye ukungu kwa kuwa yanaweza kuwa na sumu.
Kuweka kumbukumbu ni muhimu
Uwekaji wa kumbukumbu ni muhimu lakini huwa hauzingatiwi na wafugaji
walio wengi. Baadhi ya wafugaji huona kama uwekaji wa kumbukumbu ni kazi
ya ziada, ambayo kulingana na wao haina uhusiano wowote na mapato
yanayotokana na shughuli zao. Hata hivyo, bila uwekaji sahihi wa
kumbukumbu, mfugaji hawezi kufahamu ni mapato kiasi gani anayopata
kutokana na shughuli ya ufugaji. Ni kwa namna gani mfugaji anaweza
kufahamu wakati wa kumpandisha ng’ombe wake, kama hajui kuwa zimepita
siku ngapi tangu ng’ombe huyo alipozaa!
0 comments: