Kilimo Karanga: Karanga ni zao muhimu la jamii ya kunde
Ni moja ya jamii ya kunde, ambayo hulimwa lengo kubwa likiwa ni uzalishaji wa mafuta, chakula na malisho kwa ajili ya mifugo.
Karanga
ni zao maarufu sana duniani katika kilimo cha mzungunguko. Nchini
Tanzania uzalishaji wa karanga ni wa chini sana kutokana na kutokuwa na
mvua za uhakika, kiwango kidogo cha teknolojia miongoni mwa wakulima,
wadudu na magonjwa, pamoja na kutokuwa na mbegu ya uhakika.
Mmea wa karanga ni moja ya mimea mifupi ambayo huota na kuwa na urefu wa
sentimita 15-60 kwenda juu. Matunda yake huwa na kati ya mbegu moja
mpaka tano, ambapo viriba vyake huwa chini ya ardhi. Mbegu zake huwa na
kiasi kikubwa cha mafuta (38% – 50%), protini, kalishamu, potashiamu,
fosiforasi, magnesiamu na vitamini. Inasadikiwa kuwa karanga pia zina
aina fulani ya viini vinavyotumika kama dawa.
Kiasi kikubwa cha karanga inayozalishwa duniani hutumika kwa
kutengenezea mafuta ambayo hutumika kwa kupikia chakula. Makapi
yanayotokana na karanga baada ya kukamua karanga ni mazuri sana kwa
malisho ya mifugo lakini pia hutumika kwa kutengenezea unga wa karanga
ambao kwa kiasi kikubwa hutumika kwa chakula cha binadamu. Karanga pia
zinaweza kuliwa zikiwa mbichi, zikiwa zimechemshwa au kukaangwa.
Zinaweza pia kutengenezwa kama kitafunwa kwa kuchanganywa na sukari au
asali. Pia karanga hutumika kwenye supu, mchuzi, au kama kiungo kwenye
aina nyingine za vyakula kama vile nyama na wali. Mabaki ya mimea yake
ni malisho mazuri sana kwa wanyama.
Hali ya hewa
Karanga hulimwa kwenye sehemu yenye joto, wastani wa mwinuko wa mita
1500 kutoka usawa wa bahari. Kiwango cha joto kinachohitajika kila siku
ni kiasi cha jotoridi 30, na wakati wa ukuaji kinaweza kupungua mpaka
jotoridi 15. Hali ya ubaridi huchelewesha karanga kuchanua.
Udongo na kiwango cha maji
Kwa kuwa viriba vya karanga huwa kwenye udongo na ni lazima kuchimbuliwa
wakati wa mavuno, huku vikiwa ni vyepesi kuvunjika, ni vizuri kuwa na
udongo mkavu, lakini mmea hukua na kustawi vizuri kwenye udongo wa
mfinyanzi uliochanganyika na kichanga!
Mvua
Kiasi cha milimita 500-600 cha maji katika msimu wote wa ukuaji wa
karanga kinatoa fursa nzuri ya uzalishaji. Hata hivyo karanga ni moja ya
mazao yanayostahimili ukame, na linaweza kuvumiliwa ukosefu mkubwa wa
maji. Hali inapokuwa hivyo hupunguza kiasi cha mavuno.
Kupanda
Inapendekezwa kupanda kwenye sehemu ambayo udongo una kina na ambao chembechembe zake ni laini.Kuwa makini na uhakikishe kuwa sehemu ya kitalu haina magugu. Kitalu chenye udongo usiokuwa na chembe laini na tambarare inaweza kusababisha upotevu mkubwa wa mimea.
Inapendekezwa kuwa na kiasi cha mimea 200,000 – 250,000 kwenye hekari
moja, hasa kwa aina ambayo ni ya muda mfupi. Kwenye nchi nyingi karanga
hulimwa kwa kupanda kwenye mistari, ambayo mingi huwa na nafasi ya
sentimita 40 x 20 mpaka sentimita 30 x 20.
Baada ya kulima na kusawazisha vizuri, tengeneza matuta yenye mwinuko wa
sentimita 80, na sehemu ya juu iwe bapa ili uweze kupanda mistari
miwili ya karanga kwenye kila tuta. Ni lazima kuchagua mbegu za kupanda
kwa umakini. Ni lazima ziwe safi, zilizojaa vizuri na bila kuwa na
mikwaruzo yoyote.
Mbegu zinazokusudiwa kupandwa ni lazima ziachwe kwenye viriba vyake na
kumenywa siku chache kabla ya kupanda. Kina cha upandaji wa karanga ni
sawa na mahindi ambapo huwa kati ya sentimita 5-8.
Kuna aina mbili za karanga:
• Aina ya mafungu
• Aina inayotawanyika
Aina zinazolimwa Tanzania ni pamoja na Johari, Pendo, Nyota, Sawia, Mamboko.
Kupanda mseto
Karanga hulimwa kama zao linalojitegemea, lakini pia hupandwa mseto na
mahindi na hata mihogo. Ni zao zuri pia kuchanganya na mpunga unaolimwa
sehemu za mwinuko, mtama, miwa na alizeti. Ili kupata mavuno mazuri
inapendekezwa kuwa makini na nafasi tofauti na upandaji wa kienyeji. Kwa
maeneo mengine karanga hulimwa kwenye sehemu yenye miti ya mazao ya
kudumu kama vile minazi, mipapai, na miti ya mawese. Karanga
zinapopandwa mseto na mahindi kwenye sehemu zenye mwinuko husaidia
kupunguza mmomonyoko wa ardhi. Mimea ya karanga pia hupunguza uwepo wa
vidukari kwa kuwa huwa ni maficho ya wadudu rafiki. Kunakuwa na ongezeko
la mavuno ya karanga zinapopandwa mseto na kunde zinazokomaa haraka.
Matunzo
Ili kuwa na mavuno ya hali ya juu, ni lazima magugu yadhibitiwe kabisa.
Karanga ni dhaifu sana katika kukabiliana na magugu hasa katika kipindi
cha mwanzo cha ukuaji. Ni lazima palizi ifanyike mapema wakati huo miche
ikiwa inachomoza kwenye udongo. Miche ikashachomoza palizi ifanyike kwa
mikono ili kuepuka usumbufu kwa karanga changa au kuharibu maua. Palizi
ya kawaida inaweza kufanyika mpaka kwenye kipindi cha wiki 6 na palizi
ya mikono ifanyike baada ya hapo.
Virutubisho pekee vinavyohitajika kwenye shamba la karanga ni kalishamu.
Kalishamu hunyonywa moja kwa moja na viriba vya karanga endapo udongo
una unyevu unyevu. Kama kutakuwepo upungufu wa kalishamu, viriba vya
karanga vitakuwa vitupu bila kuwa na karanga. Mimea inayohitaji
Naitrojeni inaweza kupatikana kwa kushirikisha mimea mingine kama vile
kunde, badala ya kuweka mbolea ya Naitrojeni kwenye udongo.
Mavuno
Karanga
zinazokomaa kwa muda mfupi zinaweza kuvunwa kati ya siku 85-100 tangu
kupandwa, na zinazochukua muda mrefu zinaweza kuvunwa katika kipindi cha
siku 110-130 tangu kupandwa. Ng’oa mashina machache kuona kama karanga
zimeshakomaa. Karanga zilizokomaa ni lazima ziwe na rangi ya kahawia kwa
nje, ngumu na zilizokauka.
Kwa kawaida karanga zilizokomaa ndani ya kiriba huwa na rangi ya
kahawia, na hutoa sauti inapotikiswa. Magonjwa yanaposhambilia majani ya
karanga yanaweza kusababisha karanga kuvunwa kabla hazijakomaa sawa
sawa. Ni lazima karanga zichimbwe kwa umakini ili kuepuka karanga
kupasuka na kubakia ardhini. Anika kwa siku 2-3, kisha zikwanyue na
uanike tena kwenye jamvi kwa siku 7-10 ili kuondoa unyevu kufikia
asilimia kumi.
Ubambuaji
wa karanga ufanyike kwa mikono au kwa mashine maalum. Karanga
zilizopondeka, chafu au kuharibika zitengwe kwani zitapunguza ubora wa
karanga na kupunguza bei ya kuuzia. Endapo karanga hazikuhifadhiwa
vizuri zinaweza kushika unyevu unyevu ambao husababisha sumu
inayojulikana kama aflatoxin ambayo ni hatari sana kwa afya ya binadamu
hasa ini. Karanga ambazo zitatumika kwa ajili ya kupanda (mbegu) msimu
unaofuata zisibambuliwe kutoka kwenye viriba.
0 comments: