Rais wa Marekani Barack Obama na Rais Uhuru Kenyatta Kenya wamefungua rasmi kongamano la sita la kimataifa kuhusu ujasiriamali katika ofisi za umoja wa mataifa mjini Nairobi
Rais Barack Obama, kulia, na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta
"Afrika iko wazi na tayari kwa biashara" ni matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano hilo la ujasiriamali. Kwenye hotuba hiyo Rais Kenyatta amesema, "Mababu zetu walifanikiwa kushinda uhuru tunaojivunia leo lakini katika Nyanja ya kijamii na kiuchumu bara letu bado linakabiliwa na changamoto kubwa. Huu ni wakati wetu kukamilisha kazi iliyoanzishwa namababu zatuya kupigania uhuru wa kiuchumi. Ni wakati wa kizazi kipya cha Afrika kuendeleza ufanisi kwa wote."
Kwenye hotuba yake, Rais Obama ameelezea umuhimu wa kujiajiri. "Ujasiriamali unatoa nafasi mpya za kazi na biashara, njia mpya za kutoa huduma muhimu na mwelekeo mpya wa kuutazama ulimwengu. Ujasiriamali unamaanisha kujisimamia badala ya kutegemea mtu mwingine kimaisha."
Rais Obama amewachekesha wajumbe alipotamka maneno ya Kiswahili cha mtaani kinachozunguzwa hasa mjini Nairobi. "Niaje wasee. Hawayuni"
Hili ni kongamano la kwanza kuandaliwa kusini mwa jangwa la Sahara kwa sababu moja nayo ni kwamba Afrika yasonga mbele. Rais Obama amesema ujasiriamali ndio njia ya pekee ya kupambana na itikadi kali zinazopelekea ugaidi.
Viongozi hao wawili baada ya kutoa hotuba zao za ufunguzi wa kongamano hilo wameketi kwenye mdahalo na wajasiriamali na kujadili maswala ya ufumbuzi na maendeleo.
Rais Obama akiwa katika kongamano la ujasiriamali
Kongamano hilo linahudhuriwa na wajumbe wapatao 4,000 wakiwemo wajasiriamali mashuhuri kutoka mataifa 120 ulimwenguni. Zaidi ya wajasiriamali 200 kutoka Marekani waliwasili mwanzoni mwa wiki kuhudhuria kongamano hilo.
Rais Obama aliyewasili jana jioni nchini Kenya atazuru eneo la mkasa wa shambulizi la bomu la mwaka 1998 mahali palipokuwa ubalozi wa Marekani kuweka shada la maua kuwakumbuka zaidi ya watu 200 waliopoteza maisha yao kwenye shambulizi hilo.
Obama atafanya mashauri na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta kabla kukutana na viongozi wa upinzani na waakilishi wa mashirika ya kijamii.
Rais Obama ataondoka nchini kuelekea nchini Ethiopia kwa kongamano jingine la viongozi wa Umoja wa Afrika
0 comments: