BRITAM yazindua huduma zake sasa kuanza kufanya kazi nchini 

BRITAM yazindua huduma zake sasa kuanza kufanya kazi nchini 


Shirika la Britam Holdings linaloongoza katika huduma za kifedha limefanikiwa kuzindua huduma zake nchini Tanzania baada ya kukamilisha mchakato wa kuunganisha kampuni ya Real Insurance pamoja na shirika la Britam lililopo nchini Kenya.  

Uzinduzi rasmi wa shirika la bima la Britam Tanzania ni moja wapo ya mkakati wa shirika mama la Britam kukuza biashara yake ya bima na kuimarisha uwepo wake katika kanda za kusini na Mashariki mwa Afrika wakilenga makundi ya watu wasio na bima.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha usajili wa bima Tanzania ni chini ya asilimia moja la pato la taifa, kiashirio cha chini sana ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea pamoja na mataifa mengine ya Afrika. Britam inatazamia kupunguza pengo hilo kwa kuleta huduma za bima za kipekee zenye ufumbuzi wa mahitaji ya watanzania.

Britam ni shirika lenye kutoa huduma mbalimbali za kifedha na limesajiliwa kwenye soko la hisa mjini Nairobi. Shirika lina maslahi kanda nzima ya masharika na kusini mwa Afrika, likitoa huduma zake nchini Kenya, Uganda, Sudan ya Kusini, Mozambique na Malawi. Shirika linatoa huduma mbali mbali za kifedha zikiwemo bima, benki pamoja utunzaji mali.

 Akiongea jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Britam Dk. Benson Wairegi alisema kampuni hiyo itatumia uzoefu wake wa miaka 50 katika masuala ya kifedha, jina lake lina nguvu na kuaminika ndani ya nchi saba barani Afrika, nguvu kazi  kubwa ya waajiriwa wake pamoja na mfumo wake thabiti wa teknolojia.

 “Uzinduzi wa Britam nchini Tanzania ni kiashirio cha hatua muhimu iliyopigwa na shirika katika mkakati wake wa kukuza bidhaa na huduma za bima katika soko. Ndani ya Britam kuna huduma na bidhaa nyingi za kifedha katika masuala ya bima, usimamizi wa mali pamoja na benki. Wateja wetu nchini wataweza kupata huduma hizo zote chini ya paa moja,” alisema Dk. Wairegi.

Dk. Wairegi alidokeza pia jinsi Britam ni chapa inayoheshimika sana nchini Kenya, likiwa linaendesha shughuli zake kwa miaka zaidi ya 40, shirika limekuwa mstari wa mbele katika huduma wanazotoa.

Bw. Stephen Lukonyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Britam Insurance Tanzania alisema kampuni tayari ina matawi saba nchini, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma, Mbeya na Mtwara huku matawi zaidi yakiwa mbioni kufunguliwa katika siku zijazo.

 “Matawi haya yatahudumia maeneo ambayo huduma za bima bado hazijafika vya kutosha. Wananchi sasa wataweza kupata huduma zote kwa urahisi na unafuu,” alisema Lokonyo.

 Bw. Lukonyo aliongezea kwa kusema tayari kampuni wamepokelewa vizuri sana na mawakala pamoja na washika dau katika sekta ya bima Tanzania, huku akiomba kuendelea kuungwa mkono ili kuwezesha kampuni yake kutoa huduma bora kwa wateja na hivyo kusaidia kukuza soko la bima nchini.

Alisema kampuni imepiga hatua kuwa mstari wa mbele katika uvumbuzi wa bidhaa na hivi karibuni watazindua bima ya afya na usafiri katika soko la Tanzania. Kampuni pia inatazamia sekta ya mafuta na gesi pamoja na sekta ya kilimo.




Mkurugenzi Mkuu wa Britam Tanzania Bw. Stephen Lokonyo (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) katika uzinduzi rasmi wa shughuli za Kampuni ya Britam Tanzania hapa nchini ikiwa ni juhudi zinazofanywa na Britam group kujipanua kikanda. Uzinduzi huo ulifanyika juzi katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. (Kushoto) ni Mkurugenzi wa Biashara ya Bima Britam group Bw. Steven Wandera na (kulia) ni Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa Britam group Bw. Kennedy Aosa.



Meneja Mauzo wa Britam Tanzania, Bw. Godfrey Mzee (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi rasmi wa shughuli za kampuni ya Britam Tanzania hapa nchini ikiwa ni moja ya juhudi zinazofanywa na Britam group kujipanua kikanda.Mkutano huo ulifanyika juzi katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. (Kulia) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Britam Tanzania Bw. Stephen Lokonyo.



Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa Britam Group Bw. Kennedy Aosa (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi rasmi wa Kampuni ya Britam Tanzania hapa ncnini ambayo inayojishughulisha na masuala ya bima. Katika upanuzi wa soko lake Britam Group imeingia rasmi katika soko la Tanzania ambapo uzinduzi ulifanyika juzi katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi huyo aliwahakikishia watanzania kuwa lengo la Britam ni kuhakikisha kuwa inabadilisha biashara ya bima hapa nchini na kuwa chaguo la watanzania. (Kushoto) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Britam Tanzania Stephen Lokonyo.

Mgeni rasmi Jaji Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba akizindua Kampuni inayojishughulisha na masuala ya bima Britam Tanzania ambayo imeingia rasmi katika soko la Tanzania. Uzinduzi huo ulifanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam jana .Wanaoshudia ni wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo.


Mgeni rasmi Jaji (mstaafu) Joseph Sinde Warioba (katikati) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa Britam Group Dk. Benson Wairegi (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo nchini Tanzania Bw. Steven Lukonyo (kushoto) muda mfupi baada ya mheshimiwa huyo kuzindua rasmi Kampuni ya Britam Tanzania inayojishughulisha na masuala ya bima katika soko la Tanzania, uzinduzi huo ulifanyika juzi katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.



Mgeni rasmi Jaji (mstaafu) Joseph Sinde Warioba (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Britam Group Dk. Benson Wairegi (wa tano kushoto ) pamoja na wajumbe wa bodi ya Britam Tanzania muda mfupi baada ya mheshimiwa huyo kuzindua rasmi Kampuni ya Britam Tanzania inayojishughulisha na masuala ya bima katika soko la Tanzania, uzinduzi huo ulifanyika juzi katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

0 comments: