Ulimwengu unabadilika kwa kasi kubwa. Kwa hakika
jamii yoyote ambayo haijajiandaa kikamilifu kuen-dana na kasi ya mabadiliko
hayo, kuna uwezekano wa kuwa jamii yenye kutegemea misaada. Jamii hiyo
haitakuwa na mbadala zaidi ya kutembeza bakuli kwa ajili ya kuomba chochote. Na
cha kusikitisha zaidi, hali hii haitaathiri kizazi kilichopo tu, bali hata
kizazi kijacho ambacho hakitakuwa na uwezo wa kulipa madeni yaliyokopwa na baba
zao. Kwa hali hiyo, laana ya utamaduni wa kuwa ombaomba itaendelea ku-wepo kwa
vizazi hadi vizazi kwa kuwa mtoto wa ombaomba ni ombaomba pia.
Uchumi wa dunia unaonesha kuwa nchi nyingi
zilizoendelea zimeimarika katika nyanja za kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Zinaweza kuamua nini cha kufanya, jinsi ya kufanya na nini cha kufanya lini kwa
ajili ya maendeleo yao. Hali hii ni tofauti kwa nchi zinazoendelea kama
Tanzania ambazo bajeti zake kwa zaidi ya asilimia 60 hutegemea kile
kinachojulikana kama misaada ya washirika wa maendeleo (wafadhili). Nchi kama
hizo hukosa uhuru wa kufanya uamuzi.
Nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kwa
mfano, zimejaliwa raslimali ambazo zinaweza kub-adilishwa kuwa mali. Lakini
suala ni jinsi ya kuzigeuza raslimali hizo ili kuwa vitu halisi. Elimu isiyofaa
imeelezwa kuwa ndiyo kikwazo kikubwa kinachokwamisha kuzibadilisha raslimali
hizo kuwa vitu halisi. Elimu ya Tanzania inasemekana kuwa ni elimu inayowaandaa
watu kuwa waajiriwa wa maofsini, japokuwa nafasi za kazi ni chache
ukilinganisha na idadi ya watu wanaotafuta kazi za kuajiriwa. Kwa ufupi, elimu
yetu haijengi ubunifu na udadisi ambao ungewawezesha watu ama kujiajiri
(ujasiriamali) au kuzipanua fursa za ajira ambazo zingewawezesha watu wengi
kupata ajira. Fursa za ajira hazijatumiwa kwa kiwango kikubwa kiasi cha kuweza
kuwachukua watu wote wenye sifa za kuajiriwa. Chapisho hili kwa hiyo linaibua
jinsi elimu ya ujasiriamali inavyoweza kuibadilisha nchi kutoka kwenye
utegemezi na kuwa nchi yenye kujitegemea.
2.0. Maana ya Ujasiriamali
Dhana ya ujasiriamali imeelezwa kwa namna
tofautitofauti. Baadhi ya watu hufikiri kuwa ujasiriamali ni kufanya biashara
tu. Baadhi wanauangalia ujasiriamali katika muktadha mpana unaohusisha ujuzi na
maarifa ya mtu katika kutumia fursa zilizopo. Tranchet na Rienstra, (2009), kwa
mfano, wanaelezea dhana ya ujasiriamali kama uwezo binafsi wa mtu wa
kubadilisha mawazo na kuwa vitendo. Ujasiriamali unaju-muisha ubunifu,
kutengeneza kitu kipya na kuwa tayari kukabiliana na ugumu; vilevile kuwa na
uwezo wa kupanga na kuendeleza miradi ili kufikia malengo. Dhana hii humsaidia
mtu katika maisha yake ya kila siku akiwa nyumbani na katika jamii. Huwafanya
waajiriwa kuwa na uelewa kuhusu muktadha wa kazi zao na kuwa katika nafasi
nzuri katika kutumia fursa. Pia ujasiriamali hutoa msingi kwa wajasiriamali
kujenga shughuli za kijamii au kibiashara. Olomi, (2009) anakubalina na dhana
kuwa ujasiriamali kwa ujumla un-aweza kuelezewa kama namna ya kufikiri,
kutafakari na kutenda inayosababisha utengenezaji, uimarishaji, utambuzi na
ufanyaji mpya wa vitu kwa maslahi ya mtu mmoja mmoja, kikundi cha watu na
jamii.
Baadhi huelezea ujasiriamali kwa kutumia sifa za mjasiriamali. Sifa
kubwa za mjasiriamali ni pamoja na :
•
Kuwa tayari kupambana na hatari yoyote
•
Huchukua uamuzi mapema na hasubiri tatizo likue
•
Mvumbuzi
•
Mbunifu
•
Mwenye kuleta tija
•
Mwenye kujitegemea
•
Mwenye kutumia fursa zilizopo
•
Mwenye kufikia malengo yake
Kwamba, ujasiriamali ni mtazamo katika akili ya
mtu katika kutafuta fursa, kuwa tayari kukabiliana na matatizo na kuwa na uwezo
wa kutengeneza faida, kwa kuanzisha ama biashara mpya au kuongeza tija katika
taasisi. Ujasiriamali hujumuisha shughuli nyingi ikiwa ni pamoja na kuwa na
wazo, kutengeneza na kuendesha biashara. Kwamba mjasiriamali ni mtu anayefikiri
kwa ubunifu na uvumbuzi akiwa tayari kukabiliana na hatari inayoweza
kusababishwa na fursa zilizopo kwa lengo la kuzalisha faida, ajira na ustawi wa
kijamii na kiuchumi. Ujasiriamali siyo lazima uhusishe kuanzisha biashara
lakini pia kuleta tija au kubadili utamaduni wa shirika au taasisi. Wajasiriamali
huanzisha kampuni ambazo huwa injini katika ukuaji wa uchumi na utengenezaji wa
utajiri. Kompyuta, simu za mkononi, mashine za kufulia, ATM, kadi za benki na
huduma za usafirishaji ni mifano wa mawazo ya ujasiriamali yaliyobadilishwa
kuwa bidhaa au huduma.
3.0. Historia ya Elimu ya Ujasiriamali
Asili ya elimu ya
ujasiriamali katika vyuo na vyuo vikuu ilianzia Marekani ambapo kozi ya kwanza
ya MBA ilianzishwa mwaka1947 katika Shule Kuu ya Biashara ya Harvard chini ya
kichwa cha habari “Uendeshaji wa Biashara Mpya” (Katz 2003). Kuanzia miaka ya
1980 na kuendelea, elimu ya ujasiriamali ilianza kue-nea kwanza Ulaya
Kaskazini, na kisha kuenea katika sehemu za Ulaya ya Kati na Ulaya ya Kusini
katika miaka ya 1990. Elimu ya ujasiriamali baadaye ilienea katika sehemu
zingine za dunia. Kimataifa, Amerika ya Kaskazini ndio mfano wa kuigwa katika
ustawi wa miradi na pia Amerika ya Kaskazini ni kiongozi katika elimu ya
ujasiriamali. Hakuna asiyejua mchango mkubwa wa kiuchumi wa Kampuni ya
Micro-soft, Amazon, Intel, Cisco au Google na makampuni mengine yenye ustawi
mkubwa huko Marekani. Ukilinganisha na nchi zingine, Marekani ndiyo nchi yenye
historia kubwa katika elimu ya ujasiriamali, na pia ndiyo nchi yenye mpangilio,
utamaduni na mazingira rafiki ya ujasiriamali kuliko nchi yoyote duniani
(Kourilloff, 2000).
Nchini Tanzania,
elimu ya ujasiriamali haikuwepo enzi za ujamaa wakati wa Azimio la Arusha.
Wakati huo Watanzania walisadikishwa kuchukia kila kitu kinachohusiana na
ubepari, ujasiriamali ukiwemo. Mjasiriamali alichukuliwa ni kama shetani na
alilinganishwa na mnyama katili wa mwituni. Msemo “Ubepari ni Unyama” ulisikika
kwenye radio kila baada ya taarifa ya habari. Ujasiriamali uliwavutia tu wale
ambao walichukuliwa kuwa ni watu waliopotoka kimaadili. Watumishi wa umma
walizuiwa kujishughuli-sha na biashara (Rutihinda, 2002). Kwa kuwa karibu
watumishi wote wa umma walikuwa ni Waafrika, hii ina maanisha kuwa shughuli za
kibiashara zilibaki kuwa za Watanzania wenye asili ya Asia pamoja na wale
wazawa ambao walikuwa hawana ajira katika ofisi za umma. Watu wa aina hii
walikuwa ni wale ambao hawakuwa na kiwango kikubwa cha elimu (Olomi, 2009).
Hata hivyo, maendeleo ya hivi karibuni katika
ulimwengu, pamoja na sababu za ndani
zimeilazimisha nchi kuridhia mabadiliko. Baada ya kuanguka kwa ujamaa na Azimio
la Arusha, nchi ilianza kubadilika kimfumo. Mamlaka zinazohusiana na masuala ya
elimu zilianza kuiona elimu ya ujasiriamali kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi
katika miaka ya 2000 katikati. Walianza kuiweka elimu ya ujasiriamali kwenye
mihtasari yao.
4.1. Je, Wajasiriamali huzaliwa au hufundishwa?
Watu wamekuwa wakibishana iwapo wajasiriamali
hufundishwa au huzaliwa. Baadhi ya watu wanasema kuwa wajasiriamali huzaliwa.
Wanasema kwamba hakuna haja ya kuwafundisha au kuwapatia mafunzo ya
ujasiriamali watu kwa sababu mtu huzaliwa akiwa na tabia za kijasiriamali
ambazo humfanya awe mjasi-riamali moja kwa moja. Wanabainisha kuwa watu wenye
tabia au sifa za ujasiriamali hufanya vizuri katika shughuli za kijasiriamali
kwa kuwa wana tabia walizozaliwa nazo ambazo hulelewa kupitia elimu rasmi.
Wanasema kwamba cha msingi ni kupatikana kwa utamaduni wa kijasiriamali katika
jamii husika.
Hata hivyo wengine wanabainisha kuwa
ujasiriamali unasomewa. Ujasiriamali si “muujiza’, “si siri’ na hauhusiani na
nasaba ya mtu. Ni taaluma. Na kama zilivyo taaluma zingine mtu anaweza
kujifunza ujasi-riamali”. Hata hivyo swali kuwa mtu anaweza kujifunza
ujasiriamali ama la siyo suala la msingi. Kinacho-hitajika ni utamaduni
utakaoufanya uchumi wa taifa ukue (Drucker, 1985). Wajasiriamali waliofanikiwa
ni wale wenye elimu ya ujasiriamali. Egeln (2000) anabainisha kuwa utafiti
umeonesha kuwa wajasiriamali waliofanikiwa katika Bara la Ulaya ni wale wenye
elimu ya kutosha ukilinganisha na wale wasiokuwa na elimu kubwa katika
ujasiriamali. Barani Ulaya waanzilishi wengi wa miradi inayohusiana na
teknolojia mpya ni wale wenye elimu ya chuo kikuu. Utafiti uliofanyika nchini
Ujerumani umeonesha kuwa biashara zilizoanzishwa na watu wenye elimu ya kiwango
cha shahada ya kwanza, biashara zao hukua kwa haraka kuliko miradi
inayoanzishwa na watu wenye kiwango cha chini ya elimu.
Olomi, (2009) anabainisha kuwa elimu ni muhimu
kwa wajasiriamali. Aliona kwamba wale wenye elimu ya ujasiriamali hufanya
vizuri katika biashara zao ukiliganisha na wale wasiokuwa na elimu ya
ujasiria-mali. Anabainisha kuwa wajasiriamali wenye elimu ya ujasiriamali wana
uwezo wa kufanya mabadiliko makubwa katika biashara zao ukilinganisha na wale
wasiokuwa na elimu ya ujasiriamali. Anahitimisha kwa kusema kwamba katika
biashara kitu cha msingi si kiwango cha elimu aliyonayo mtu bali ni uwezo wake
wa kutimiza malengo pamoja na ufanisi katika mchakato wa elimu. Tranchet na
Rienstra (2009) wanasema kwamba katika nchi nyingi, utamaduni na ukosefu wa
uelewa katika ujasiriamali vinaweza kuwa vikwazo katika ubunifu na ukuaji wa
uchumi. Kwa kuongeza maarifa na kujenga ujuzi muhimu katika ngazi zote za
elimu, kizazi kipya chenye mawazo ya ujasiriamali kinaweza kuubadilisha na
kuukuza uchumi wa dunia.
Wanafunzi wanaojikita katika fani ya
ujasiriamali huwa si watu wa kukubali kila kitu, huwa si watu wenye kujiangalia
wao tu, ni watu wenye utayari wa kupambana na hatari yoyote, ni watu wanaokaribisha
mab-adiliko, wana nguvu katika kiwango cha juu, wana sifa kama zile za
wajasiriamali waliofanikiwa (Sexton na Browman, 1985). Pia, tafiti zinaonesha
kuwa wale wanaochukua kozi za ujasiriamali wana uwezekano mkubwa wa kuanzisha
biashara ukilinganisha na wale ambao hawasomi kozi za biashara (Vijverberg,
1984; Bird, 1989 katika Olomi, 2009).
Ulimwengu umekuwa kama kijiji. Ili kuweza kudumu
katika utandawazi, mtu anapaswa kuwa na maarifa ya kutosha ili aweze kuishi
katika ulimwengu huu. Ulimwengu umeshuhudia mafanikio makubwa katika biashara.
Mafanikio hayo yanahusishwa na utamaduni wa watu wake ambao unawahamasisha
wajasiria-mali kukuza uchumi wa taifa. Kwa maneno mengine, elimu ya
ujasiriamali hujenga utamaduni wa kijasi-riamali katika akili za watu, na hivyo
ni muhimu kwa maendeleo ya wajasiriamali.
3
5.0. Malengo ya elimu ya ujasiriamali
Kama ilivyo katika fani zingine, Elimu ya
ujasiriamali ina malengo yake. Kwa mfano malengo makuu ya elimu ya ujasiriamali
katika vyuo na vyuo vikuu vya Marekani kwa kawaida ni kuendeleza uwezo wa
ki-jasiriamali katika akili za walengwa na kukuza utambuzi wa kijamii katika
mikakati inayohusu ujasiriamali (Tume ya Ulaya, 2008).
Tanzania imejaliwa raslimali nyingi. Ni kama
ndiyo kitovu cha raslimali duniani. Lakini changamoto ni jinsi ya kuzigeuza
raslimali hizi ili ziweze kuleta tija na kutumika kama inavyostahili ili ziweze
kumnufaisha mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla. Kushindwa kuzibadili raslimali
hizi kunatokana na kuwa na maar-ifa na ujuzi kidogo katika kutambua nafasi ya
elimu ya ujasiriamali. Watu wengi hufikiri kuwa ujasiriamali hauhusiani na
elimu: Kwamba kila mtu anaweza kufanya shughuli za kijasiriamali bila kuwa na
semina au mafunzo juu ya ujasiriamali. Hii si sahihi. Malengo ya elimu ya
ujasiriamali yanajumuisha mabadiliko katika mtazamo wa watu ili wawe
wajasiriamali katika maeneo yao ya kazi: kutatua tatizo la ajira kwa ku-zalisha
watengeneza kazi miongoni mwa wasomi: kugundua na kutumia fursa zilizopo kwa
maendeleo ya mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla; kuiona dunia kama fursa na
wala si sehemu mbaya ya kuishi.
6.0. Hali ya Elimu ya Ujasiriamali nchini Tanzania
Kama zilivyo nchi zingine ambazo zimepitia hatua
mbalimbali katika maendeleo, Tanzania pia imepitia hatua mbalimbali katika
mabadiliko ya mfumo. Baada ya miaka saba tu ya uhuru, iliridhia kuwa na mfumo
wa ujamaa katika maendeleo yake. Vilevile, mfumo wa elimu ulikuwa wa kijamaa.
Nchi ilijenga elimu ya kujitegemea ambapo mtu aliandaliwa kujitegemea katika
maisha yake ya baadaye. Kusema kweli, falsafa hii ilikuwa nzuri kwa ustawi wa
watu. Kwa kuangalia maudhui ya falsafa, Elimu ya Kujitegemea ililenga katika
kuzalisha watengenezaji wa ajira badala ya watafuta ajira ambayo pia ndiyo
malengo ya elimu ya ujasiriamali. Hata hivyo, kwa kuwa wafanyabiashara
walichukuliwa kama watu waliopotoka kimaadili na hawakuwa na elimu kubwa elimu
ya ujasiriamali haikupewa msisitizo. Rutihinda (2002) kwa mfano, amebainisha
kwamba nchini Tanzania, enzi za ujamaa, Watanzania walisadikishwa kuchukia
karibu kila kitu kinachohusu ubepari. Mjasiriamali alichukuliwa kama shetani na
alifananishwa na mnyama mkali wa mwituni. Msemo kama “Ubepari ni Unyama”
ulisikika kwenye radio kila baada ya taarifa ya habari. Ujasiriamali ulionekana
kufaa kwa wale tu waliopotoka kimaadili ambao wana uelewa mdogo. Watumishi wa
umma walipigwa marufuku kujishughulisha na biashara.
Baada ya kuanguka kwa mfumo wa ujamaa na elimu
ya kujitegemea, Tanzania haikuridhia ujamaa wala ubepari. Hata hivyo, katiba ya
taifa inatamka wazi kuwa Tanzania ni nchi ya kijamaa inayofuata sera ya ujamaa
na kujitegemea ingawa kiuhalisia ni nchi ya kibepari. Huduma za jamii kama
elimu na afya kwa sasa ni za kulipia na siyo bure tena kama zilivyokuwa hapo
mwanzoni. Kwamba, hata muundo na maud-hui ya elimu yamebadilika kutoka kwenye
mfumo wa elimu ya kujitegemea na kuwa kitu kingine katika kipindi hiki cha soko
huria na ubinafsishaji. Hakika, sera na mtaala mpya umeandaliwa na kuwekwa
kwe-nye utekelezaji. Kuanzishwa kwa Sera ya Elimu ya Juu, sera ya TEHAMA katika
shule za msingi, Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na vya Kati, kwa uchache
tu ni mifano bayana ya sera zinazoendana na ubinafsishaji na soko huria.
Sera ya Elimu ya mwaka 1995 ambayo ndiyo mama wa
sera zingine zote katika ngazi zote za elimu haisemi chochote kuhusu elimu ya
ujasiriamali. Inatilia mkazo maarifa na ujuzi utakaomfanya mlengwa ajitegemee
baada ya kumaliza mafunzo yake.
Sera ya elimu ya juu inatilia mkazo kuhusu elimu
itakayotolewa kwa wanafunzi na ambayo itawapatia maarifa na ujuzi
utakaowawezesha kujiajiri. Mihtasari ya vyuo vikuu inatofautiana sana. Hakuna
mfanano
4
wa mambo yanayotakiwa kufundishwa katika vyuo
vikuu vilivyosajiriwa nchini Tanzania. Kila chuo kikuu huandaa kozi na maudhui
kwa kufuata taratibu na falsafa yao. Matokeo yake, kila chuo kikuu hutumia
uzoefu wake katika kupanga na kufundisha somo husika. Kwamba kukosekana kwa
mfanano juu ya kile ambacho kinatakiwa kufundishwa na jinsi ya kufundishwa, na
kile ambacho kimepewa baraka na Tume ya Vyuo Vikuu huzidi kuongeza ukubwa wa
tatizo.
Vyuo vikuu vingi hufundisha ujasiriamali. Cha
kushangaza, hufundisha ujasiriamali kama mada au mada ndogo ambayo hujumuishwa
katika Taaluma ya Maendeleo. Katika vyuo au vyuo vikuu vingine nchini Tanzania
ujasiriamali hufundishwa kama somo la hiari! Hata vile vyuo vikuu ambavyo hutoa
mafunzo ya uzamili, vyuo vingi hujumuisha ujasiriamali katika shahada ya
Uzamili katika Uongozi wa Biashara, lengo likiwa ni kuwapatia wanafunzi
utamaduni wa ujasiriamali utakaowawezesha kuongoza taasisi zao kwa kufuata
utaratibu wa kijasiriamali. Pia ujasiriamali hufundishwa kama mada kuu au mada
dogo. Hata vile vyuo au vyuo vikuu vichache ambavyo vimeanzisha mafunzo ya shahada
za uzamili au stashada za kawaida na za juu katika ujasiriamali vimekuwa
vikipanga kozi kwa kufuata utaratibu wao; wakati mwingine vikikosa mwelekeo
katika somo. Ndiyo maana baadhi ya vyuo na vyuo vikuu hufundisha ujasiriamali
kama mojawapo ya vigezo vya uzalishaji au somo linalohusu uendeshaji wa
biashara (biashara za mitaani) tu! Mbaya zaidi, somo hufundishwa na watu ambao
hawana maarifa ya kutosha kuhusu somo. Vyuo vikuu vingi huajiri watu wenye
shahada za uzamili za MBA ambao hufanya kazi kama wahadhiri wasaidizi. Hawana
uelewa kuwa watu wenye shahada za MBA wana elimu ndogo ya ujasiriamali na hivyo
wanawanyima wanafunzi haki ya kupata elimu bora ambayo wanastahili kuipata.
Katika shule za sekondari hali ni mbaya
vilevile. Muhtasari wa elimu ya sekondari hausemi chochote kuhusu elimu ya
ujasiriamali. Katika ngazi za juu za elimu ya sekondari, ujasiriamali
unachukuliwa kama kigezo cha uzalishaji kwa wanafunzi wa kidato cha tano na
sita wanaosoma somo la uchumi. Pia katika Masomo ya Jumla, ujasiriamali
hauchukuliwi ama kama mada kuu au mada ndogo. Wanafunzi wengi wa sekondari
wanaomaliza elimu yao hawaelewi chochote kuhusu ujasiriamali kama taaluma bali
husikia tu kuwa ujasiriamali unahusishwa na biashara ndogondogo za mitaani!
Muhtasari wa elimu ya msingi hausemi chochote
kuhusu elimu ya ujasiriamali. Huzungumzia kuhusu maarifa ya jamii ambayo
yamelenga kuwapatia wanafunzi maarifa na ujuzi wa kuwa wabunifu na wavum-buzi.
Hata hivyo walimu wanaofundisha maarifa ya jamii hawana maarifa ya kutosha kuwawezesha
wana-funzi wawe wa uwezo wa ziada wa kufikiria. Kwa kawaida wanatilia mkazo
katika utengenezaji wa vyungu na upambaji na kazi zingine zinazofanana na hizo
na ambazo zimekuwa ndiyo utaratibu wa maisha ya kila siku. Wanakosa mbinu na
ujuzi wa kuwafanya wanafunzi wafikirie na kubuni mambo yasiyo ya kawaida.
Ukosefu
wa elimu ya ujasiriamali kwa shule za msingi ni miongoni mwa sababu za kuandaa
watafuta kazi badala ya watengeneza kazi.
7.0. Athari za Kukosekana Msisitizo kuhusu Elimu ya Ujasiriamali
Nguvu ya ujasiriamali imethibitisha kuwa yenye
matokeo makubwa katika nchi nyingi ambazo huchu-kulia elimu ya ujasiriamali
kama ndiyo inayotengeneza kazi, injini katika ukuaji wa uchumi na silaha ya
kupambana na umasikini kwa uchache tu. Kourilloff (2000) anabainisha kwamba
hakuna anayeweza kuhoji mchango mkubwa wa kiuchumi wa kampuni ya Microsoft,
Amazon, Intel, Cisco au Google na makampuni mengine makubwa nchini Marekani
ambayo ni matokeo ya wajasiriamali. Kwamba kwa kulinganisha na nchi zingine,
Marekani ndiyo nchi yenye historia ndefu katika elimu ya ujasiriamali, na pia
miongoni mwa nchi zenye utamaduni rafiki juu ya ujasiriamali duniani. Marekani
imejipambanua kuwa ni nchi inayoongoza katika ubunifu na uvumbuzi kuliko nchi
zote.
Ukweli ni kwamba iwapo nchi haitatilia mkazo
elimu ya ujasiriamali itasababisha kuwa na tatizo la ajira, ukuaji mdogo wa
uchumi, umasikini na upeo mdogo wa kufikiri kwa watu wake. Elimu ya
ujasiriamali huchangia katika ukuaji wa uchumi. Imegundulika kuwa wajasiriamali
wa ndani huchangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa (GDP). Kwa mfano,
mtu anapaswa kujiuliza kuhusu mchango wa Makam-puni ya IPP au Bakhresa katika
uchumi wa taifa hasa kwa kuzingatia mapato ambayo nchi hupata kupitia (kodi) na
utengenezaji wa ajira, achilia mbali mchango wa makampuni hayo katika
upatikanaji wa huduma za jamii. Iwapo elimu ya ujasiriamali haitatiliwa mkazo,
nchi itakuwa tegemezi kwa bidhaa za nje na hivyo kushindwa kupiga vita ujinga,
maradhi na umasikini.
8.0. Mahitaji ya Elimu ya Ujasiriamali yenye Ufanisi nchini Tanzania
Elimu ni mchakato usioisha wa upataji maarifa.
Mtu anaweza kupata maarifa kwa njia rasmi au isiyo rasmi. Elimu rasmi ni ile
tunayoipata kutoka kwenye taasisi za elimu kama vile mashule. Elimu isiyo rasmi
ni aina ya elimu ambayo haimlazimu mtu kwenda shule. Inaweza kupatikana muda
wowote na popote. Lengo kubwa la elimu ni kutengeneza maisha bora kwa watu.
Tunapozungumzia elimu ya ujasiriamali
tunamaanisha elimu inayotilia mkazo katika kufikiri kwa ubunifu katika kutumia
fursa zilizopo kwa lengo la kutengeneza ajira ambazo husaidia katika ustawi wa
kijamii na ukuaji wa uchumi. Hii ndiyo aina ya elimu ambayo inaweza kuyafanya
maendeleo ya taifa kuwa endelevu. Maendeleo endelevu ni aina ya maendeleo
yanayokidhi mahitaji ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho. Ni aina ya maendeleo
ambayo hayatikisiki upesi bali yanaweza kudumu na kuhimili vikwazo vya, kijamii
ki-siasa na kiuchumi.
Nchini Tanzania elimu ya ujasiriamali inahitajika
sana ili kuzitumia kwa ufanisi fursa na raslimali zilizopo. Tanzania imejaliwa
maziwa, mito, bahari, mabwawa n.k. ambayo siyo kwamba yamejaa samaki tu bali
yamejaa pia viumbe wengine kama vile viboko, mamba n.k. Nchi imejaliwa ardhi
kubwa ambayo haijatu-mika, misitu na wanyama mwitu na wale wa kufugwa. Pia nchi
imejaliwa kuwa na gesi na madini kama vile almasi, dhahabu, Tanzanite, makaa ya
mawe kwa uchache tu. Hata hivyo, vitu vyote hivi havijatumiwa kikamilifu ili
kuleta maendeleo ya watu. Kwa maneno mengine, tunakosa maarifa na ujuzi wa
kiujasiria-mali katika kuzibadilisha fursa hizo kuwa maendeleo. Iwapo tunataka
maendeleo endelevu lazima tuten-geneze/tuandae watu ambao wanaweza:
•
Kuendeleza bidhaa mpya
•
Kugundua huduma na njia mpya zinazotilia mkazo
matumizi halisi katika kiwanda au shirika
•
Kugundua na kutumia masoko mapya ambayo kiwanda
au shirika halijayatumia
•
Kugundua na kutumia nyenzo mpya za utoaji
raslimali ambazo hazijawahi kutumika
•
Kuwa tayari kupambana na hatari yoyote kwa faida
ya nchi
Nchini Tanzania tunahitaji watu ambao wanaweza kuleta tija katika
uzalishaji kwenye taasisi au mashirika.
Utafiti uliofanyika hivi karibuni umeonesha
kwamba huduma za afya nchini Tanzania ni duni sana. Kwa mfano, asilimia 53 ya
wagonjwa wanaofika hospitalini huhudumiwa baada ya kusubiri kwa muda wa masaa
mawili au matatu na asilimia 19 ya wagonjwa ambao hufikishwa hospitalini
huombwa rushwa.
Haya yote hutokea kutokana na kukosekana kwa
elimu ya ujasiriamali. Hawaijali raslimali watu na wanadhani kuwa uzalishaji
unaweza kupatikana kwa njia ya hongo. Ili kuleta ufanisi na tija katika
upatikanji wa huduma na bidhaa, taasisi au shirika lolote linapaswa
kuwajumuisha wajasiriamali ambao wanaweza kuleta tija kwenye huduma na bidhaa
kwa lengo la kuongeza uzalishaji.
Pia tumeshuhudia kushuka kwa ubora wa elimu
kunakoendana na matokeo yasiyoridhisha kwa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari nchini Tanzania. Mengi yamesemwa kuhusu suala hilo. Mambo hayo
yanajumuisha miundombinu isiyoridhisha na vifaa visivyoridhisha vya kufundishia
na kujifunzia. Hata hivyo kuna sababu nyingine ambayo huwa tunaisahau. Sababu
yenyewe ni kwamba tunakosa ubunifu na uvumbuzi miongoni mwa walimu na wanafunzi
katika michakato ya ujifunzaji na ufundishaji. Wanatumia njia za zamani za
ufundishaji na ujifunzaji. Juhudi za kugundua njia mpya za ufundishaji na
ujifunzaji ni ndogo. Kinachosababisha hali hii ni ukosefu wa utamaduni wa
kijasiriamali ambao unaweza kubadili mtazamo wa mtu katika kukabiliana na
ulimwengu. Wakati walimu na wanafunzi katika nchi zingine wakijaribu kuvumbua
na kubuni njia mpya za ujifunzaji na ufundishaji, sisi bado tuna-shikilia njia
za zamani za ujifunzaji, ufundishaji na upimaji wa wanafunzi wetu. Matokeo
yake, baadhi ya wanafunzi (wakati mwingine, kwa kushirikiana na walimu wao)
wanafanya udanganyifu katika mitihani. Pia ukweli uliodhahiri ni kwamba
kutokujua kusoma na kuandika kunaongezeka. Kwa mfano, kulikuwa na wanafunzi 308
wa Kidato cha Kwanza wasiojua kusoma na kuandika katika kata ya Nansimo katika
wilaya ya Bunda. Pia, mkoa wa Arusha unaongoza katika udanganyifu kwenye
mitihani. Unaongoza kwa asilimia 48. Pia ilibainika kwamba ni asilimia 14 tu ya
wahitimu wa shule za msingi walifaulu mtihani wa hisabati mwaka jana. Hali hii
kwa mujibu wa utafiti ilitokana na ukosefu wa uvumbuzi na ubunifu miongoni mwa
walimu wa hisabati katika kulifanya somo hilo lieleweke vizuri. Pia ukosefu wa
mbinu zinazowapatia wanafunzi motisha ya kulipenda somo la hisabati huchangia
katika ufaulu duni wa wana-funzi. Iwapo walimu wangefundishwa kuhusu
ujasiriamali (ujasiriamali wa mashirika), hali hii ingekuwa imepungua kama siyo
kuondolewa kabisa.
9.0. Nini kifanyike?
Ili kuwa na elimu ya ujasiriamali yenye ufanisi
kwa ajili ya maendeleo endelevu ya mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla, mambo
yafuatayo inabidi yafanyike:
•
Mihtasari/programu
na moduli za elimu ya ujasiriamali ni lazima ziwe na malengo ya kuendeleza ari
ya ujasiriamali kwa wanafunzi (kujenga motisha na ufahamu). Hii inajumuisha
kuendeleza uwezo wa kijasiriamali ili kuweza kubainisha na kutumia fursa
zilizopo, kuwapatia wanafunzi ujuzi unaohitajika katika kuanzisha biashara na
kuziendesha ili zikue. Katika hali hizi zote, ni muhimu kuwahamasisha wanafunzi
ili waweze kufikiri na kutenda kama wajasiriamali na pia ili wawe we-nye
kuwajibika kimaadili na kijamii.
•
Ujasiriamali ni
sharti ufundishwe na wataalamu ambao wanafahamu jinsi ya kulifundisha somo
hili. Inapaswa kufahamika kwamba ujarisiarimali ni vitendo na kwamba ili
kuwapatia motisha wa-nafunzi, njia/mbinu mbalimbali za kufundishia inabidi
zitumike. Kwa mfano, ni muhimu somo la ujasiriamali lifundishwe na
wajasiriamali wenye moyo wa kufanya hivyo. Mbinu ya kuiga ni muhimu zaidi
katika ufundishaji wa ujasiriamali kwa sababu watu hupenda kumsikiliza yule
wa-nayemwamini na yule aliyefanya kitu kwenye jamii.
•
Shule ni sharti
zifungamanishwe na kazi. Uhusiano huu wa shule na kazi husaidia kupunguza
matarajio ya kazi kwa vijana na pia husaidia kupunguza tatizo la ajira kwa
wasomi walioajiriwa na wale wasio na ajira.
10.0. Hitimisho
Elimu ya ujasiriamali si ya zamani kama zilivyo
fani nyingine kama vile sayansi ya siasa, falsafa na sosholo-jia, lakini
ujasiriamali umeleta mabadiliko makubwa tangu kuanza kwake. Kompyuta, mashine
za ATM, simu za mikononi, kwa uchache tu ni bidhaa zinazotokana na
ujasiriamali. Ijapokuwa mtu anaweza kuwa na sifa za ujasiriamali, ni sharti
afundishwe somo hilo ili kumpatia maarifa na ujuzi wa kushindana katika
ulimwengu kwa ujumla wake. Ufundishaji makini wa ujasiriamali utawezesha
kupatikana kwa maendeleo endelevu na hivyo kuwawezesha watu kuwa na maisha
mazuri katika nchi zao.
0 comments: